JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Tarime na Rorya Mkoani Mara,
kupitia askari wake wa FFU limelazimika kutumia nguvu pamoja na
kuwatisha kwa silaha wananchi na waombolezaji wa marehemu, Mgosi Magasi
Chacha (30), aliyekufa baada ya kupigwa risasi ya moto na polisi
wanaolinda mgodi wa North Mara uliopo Wilayani hapa.
Katika tukio hilo la leo Jumatano saa 5:10 asubuhi, polisi wakiwa
kwenye magari manne huku wakiwa wamebeba silaha ikiwamo bunduki aina ya
SMG, mabomu ya machozi na marungu, waliwasili kwenye hospitali ya wilaya
ya Tarime kuchukuwa mwili wa marehemu Chacha kwa nguvu ili kwenda
kuuzika baada ya kuwakamata baadhi ya viongozi wa Chama cha Demokrasia
na Maendeleo (Chadema) waliokuwa katika msiba huo.
Mgodi wa North Mara unamilikiwa na kampuni kubwa ya uchimbaji madini
duniani ya Barrick Gold, na umekuwa katika mgogoro na wenyeji wa eneo
hilo mara kwa mara hali inayosababisha kuwapo kwa matukio
yanayohatarisha amani mara kwa mara.
Wakati polisi hao wa FFU waliokuwa wametanda aneo kubwa la hospitali
hiyo wakitaka kuchukua mwili wa marehemu, mamia ya wananchi, ndugu wa
marehemu akiwemo mkewe (jina lake halikupatikana), pamoja na viongozi wa
Chadema wilaya ya Tarime, waliwazuia polisi kuuchukuwa mwili huo,
wakitaka lazima taratibu za kisheria zifuatwe na si vinginevyo.
Baada ya viongozi hao wa Chadema, wananchi, ndugu na jamaa wa
marehemu Chacha kuchachamaa, mke wa marehemu alikuwa akilia kwa uchungu
huku akiwa amekaa karibu na mlango wa chumba cha kuhifadhia maiti,
akikataa polisi kuchukuliwa mwili wa mumewe kwenda kuuzika bila ndugu na
yeye kuridhia, lakini askari kanzu mmoja wa kiume alionekana kuanza
kumburuza mke huyo wa marehemu kwa lengo la kumtoa eneo hilo ili polisi
wachukuwe mwili huo.
Wakati mke huyo wa marehemu akiburuzwa na mmoja wa askari polisi
aliyekuwa akitii amri ya mkubwa wake wa kazi (majina hayakupatikana),
mwanamke huyo alikataa katakata kuondoka, lakini polisi nao walionekana
kumlazimisha hadi baadhi ya nguo zake alizokuwa amejifunga zikidondoka
kisha baadhi ya maeneo ya mwili wake juu ya kiuno yakiwa yanaonekana
nje, jambo ambalo lilioelezwa na walioshuhudia kama ni udhalilishaji.
Mwandishi wa habari hizi alishuhudia vurugu hizo, baina ya polisi na
ndugu wa marehemu, ambapo polisi walilazimika kuweka chemba risasi za
moto katika bunduki zao za SMG, baada ya kuona wametaka kuzidiwa nguvu,
ambapo waliwakamata na kuwaweka ndani mwenyekiti wa Chadema wilayani
Tarime, Lucas Ngoto.
Viongozi wengine wa Chadema waliokamatwa na polisi katika tukio hilo
ni, Katibu wa Chadema wilaya hiyo, Mroni Mwita pamoja na diwani wa Kata
ya Sabasaba, Christopher Chometa, huku mwenyekiti wa Baraza la Vijana
Chadema (Bavicha), wilaya ya Tarime, Chacha Heche akiponea chupuchupu
kukamatwa kwa madai ya kutaka kuzuia mwili huo wa marehemu usiondolewe
hospitalini hapo kwenda kuzikwa.
Marehemu Chacha mkazi wa Kijiji cha Nkende ambaye alikuwa mwendesha
pikipiki wilayani Tarime, aliuawa Juni 4 mwaka huu majira ya saa 1:45
asubuhi, kwa kupigwa risasi ubavuni kisha kutokea tumboni na askari
polisi wanaolinda mgodi huo wa North Mara, unaomilikiwa na kampuni ya
Barrick, na kwamba jeshi la polisi Kanda maalumu ya Tarime na Rorya
imethibitisha askari wake kumuua raia huyo, bila kutaja sababu ya mauaji
hayo.
Hata hivyo, baada ya vuta nikuvute hiyo iliyodumu takribani dakika
45, hatimaye polisi walifanikiwa kuuchukuwa mwili huo wa marehemu Chacha
na kuuondoa nao hospitalini hapo ukiwa chini ya ulinzi mkali wa polisi,
na kwamba magari yaliyokuwepo eneo hilo yakiwa yamesheheni askari ni PT
2036, PT 1873, PT 1863, T 754 BLF pamoja na pikipiki moja ya doria,
huku gari la halmashauri ya wilaya hiyo SM 5241 ndilo lililotumika
kuubeba mwili huo wa marehemu.
Taarifa ya jeshi la polisi Kanda hiyo maalumu, iliyotolewa na Kaimu
Kamanda wa Kanda hiyo ya Kipolisi, Sebastian Zacharia-SSP ilieleza
kwamba awali marehemu alijeruhiwa kwa risasi tumboni na askari polisi,
kwa madai ya kumkata panga mguu wa kushoto mlinzi mmoja wa mgodi huo,
Winchlaus Petro (26).
“Kabla mauti kumkuta alijeruhiwa kwa kupigwa risasi tumboni na askari
polisi waliokuwa doria eneo hilo la mgodi. Marehemu alianza
kumshambulia askari kwa panga na kuikata silaha ya askari huyo mara
mbili hata baada ya kuonywa kwa kupiga risasi hewani wakati wa
kukamatwa”, ilisema sehemu ya taarifa hiyo ya polisi yenye kurasa moja.
Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo ya wilaya ya Tarime, Nagga Marco
ilisema, uchunguzi wake umebaini marehemu Chacha alipigwa risasi ubavuni
karibu na mgongo, kisha risasi hiyo ikatokea tumboni.
Kwa upande wao familia na ndugu wa marehemu huyo, akiwemo baba yake
mkubwa, Charles Matiko waliieleza FikraPevu kwamba, nguvu iliyotumiwa na
polisi kuchukuwa mwili wa kijana wao ni ya kinyama, kwani familia
ilikuwa haijaridhia kuchukuliwa kwa marehemu kutokana na ukweli kwamba
mipango ya maziko ilikuwa haijakamilika.
Mauaji ya watu eneo hilo la mgodi wa Nyamongo, yanaelezwa kushamiri,
ambapo inadaiwa mwaka jana vijana wapatao watano waliuawa kwa kupigwa
risasi na polisi, Mei 7 mwaka huu kijana mwingine aliyetajwa kwa jina
moja la Mwikwabe aliauawa eneo hilo la mgodi, na kwamba Juni 4 mwaka huu
marehemu Chacha aliuawa pia kwa kupigwa risasi ya moto na askari polisi
wanaolinda mgodi huo wa North Mara ambao unamilikiwa na kampuni ya
kigeni ya Barrick.
Habari imeandaliwa na Sitta Tumma, Tarime
No comments:
Post a Comment