NDOA! Ni neno lenye herufi nne tu, lakini tafsiri yake ni kubwa, iliyojitanua katika mawanda mapana na matawi lukuk Ndoa ni taasisi kubwa na ya kwanza, kabla ya zote iliyoanzishwa na Mungu.Katika kitabu cha Mwanzo Sura 2: 24 Biblia inasema:
“Kwa sababu hiyo mwanaume atamwacha baba yake na mama yake ataungana na mkewe na hawa wawili watakuwa mwili mmoja.”
Mchungaji James Dobson kutoka England anaitafsiri ndoa kama zawadi muhimu ya kudumu wanadamu waliyopewa na Mungu.
Mimi si mtaalamu wa masuala ya uhusiano, lakini yaonekana dhahiri kuwa, ndoa siku hizi zimepoteza maana yake.
Ndoa imegeuka na kuwa si wito na kiapo kitakatifu tena, bali imegeuka na kuwa ni mtindo wa maisha.
Maana nzima ya ndoa imebadilika na hapa kila mmoja anakuja na sababu yake ya kuingia katika taasisi hii.
Wengi wanaingia si kwa mapenzi ya kweli, si kwa kuviishi viapo vyao, bali kwa maono yao binafsi tena ya kibinafsi.
Wengine wamekuwa wakifunga ndoa ili wapate zawadi za vyombo katika sherehe za kufundwa au zile za harusi. Wengine wanakiri kabisa, kuwa, “Niliamua nimuoe kwa sababu alikwishashika mimba.”
Baadhi, huoa au kuolewa kwa sababu tu, “mwenza ana kipato” hivyo anajua hatapata shida ndogo ndogo.
Lakini, tujiulize hii kweli ndiyo maana ya ndoa?
Mwanamke
na mwanaume wanaooana, aghalabu hula viapo kuwa watakabiliana na yote
yatakayowakuta katika maisha yao. Iwe ni furaha, huzuni, shida, raha,
katika ugumba, iwe ni watoto wengi, katika uzee na maradhi.
Ajabu ni kuwa viapo hivi huwa ni vya mdomoni tu na si ajabu kusikia mwanandoa kamtelekeza mwenza wake baada tu ya kuanza kuugua au kufukuzwa kazi.
Sio siri kuwa ndoa zimekuwa nyingi mno siku hizi. Kengele za harusi hugongwa kila kukicha.
Lakini, ukweli ni kwamba, nyingi zimefunikwa na migogoro … zikitembea kwa mahadhi ya kutoaminiana, huku mawimbi ya usaliti yakiwasonga wanandoa. Na mwishowe huvunjika.
Usifikiri ni hadithi, kusikia kuwa bwana
harusi alifanya mapenzi na mwanamke mwingine, siku moja kabla ya harusi
yake.Si ajabu siku hizi kusikia kuwa, bibi harusi mtarajiwa, kakutwa
anafanya biashara ya kuuza mwili viwanja vya Ohio.
Ndiyo maana
tunasema ndoa za siku hizi si wito, ni mtindo wa maisha ambao wahusika
huujaribu mtindo huo, aidha waonekane nao waliupitia(wasipitwe na
wakati) au wanaujaribu kama utawafaa.
Wakati mwingine wanandoa huingia ndoani ili kuwaridhisha wazazi, ambao pengine wanataka mkwe kwa wakati huo.
Maono ya ndoa yanaonekana kuwa yapo mbali mno na wanandoa wenyewe kama zilivyo sayari mbili za Mars na Venus. Wanachokifanya sicho kinachotakiwa ndoani.
Yumkini viongozi wa dini wanashindwa kuwa wakali katika hili au kuweka msisitizo bayana kuhusu kuiheshimu ndoa.
Yawezekana wazazi wameshindwa pia kutilia mkazo umuhimu wa kuithamini taasisi hii.
Lakini kubwa zaidi linaloonekana ni kuwa … hofu ya Mungu haipo.
Woga
wa kumsaliti mume au mke umetoweka kabisa. Maana yake ni kuwa, ndoa
imegeuka na kuwa si ya watu wawili, lakini yenye matawi kadhaa yasiyo
rasmi.
Mchungaji mmoja aliwahi kuwaasa wanandoa fulani wapya kwa maneno muhimu mno.
Aliwaambia:
“Iweni wakarimu kwa watu wote na hasa kwa majirani zenu ili watu
wawaombe moto au maji ya kunywa, lakini kamwe msiwe wakarimu katika
vitanda vyenu vya ndoa."
Ingawa takwimu rasmi hazijapatikana, lakini idadi ya mabinti waliozaa na waume za watu ni kubwa.
Mabinti hawa, wamekubali kwa radhi ya mioyo yao, kuzaa na waume za watu wakidai kuwa, wataishi maisha huru, tofauti na ndoani.
Swali linaloibuka hapa ni, je, kwa nini wanaume hawa wamezisaliti ndoa zao?
Dini zote duniani hazikubali uzinzi huu, dini ya Kiislamu inaruhusu mke wa pili, lakini kwa kufuata sheria zote. Wapo pia wake za watu, ambao hudiriki kutembea nje ya ndoa zao.
Upepo
huu umewachota hata vjana wadogo ambao tunawaita ‘Kizazi Y’, Ile hofu
ya binti au kijana kuwa na uhusiano na mume au mke wa mtu … haipo tena.
Licha ya usaliti wa kutisha katika ndoa, lakini katika nchi zilizoendelea, siku hizi ndoa ni za kimkataba.
Kwa mfano, wanandoa wanamuziki, Beyonce na Jay Z, wameoana kwa mkataba. Mkataba huo wa miaka miwili miwili unasema, endapo mwenza mmojawapo atamwacha mwenzake, kabla ya mkataba, basi atamlipa dola milioni kumi.
Je, kuishi kwa mikataba ndiyo maana halisi ya ndoa? Mkataba huu una mapenzi ya kweli au ni wa kimaslahi zaidi?
Kama wanandoa wanaishi kimkataba, unadhani viapo wanavyokula mbele ya mchungaji, padre au sheikh ni vya dhati ya mioyo yao?
Baya
zaidi ambalo limeibuka miaka ya karibuni ni ndoa za jinsia moja.
Wanaharakati wanaozitetea ndoa hizi, wanavitumia vibaya vipengele muhimu
kwa wanandoa na kuvihalalisha katika ndoa hizi.
Lakini, vitabu
vya dini vinawataja wanandoa kuwa ni ‘Adam na Hawa’ na si Asha na Rose
au Juma na Yussuf. Katika taasisi hii ya watu wawili aghalabu
tunatarajia matunda ambayo ni watoto yaonekane. Lakini ndoa za jinsia
moja zitaletaje matunda hayo?
Usemi wa ‘ndoa ndoano’ unazidi
kupata umaarufu. Hili linatafsiri hasi kwa taasisi hii, inaonyesha
kabisa kuwa imekosa mwelekeo- imelewa kama machela.
Viongozi wa dini wanahitaji kufanya kazi ya ziada ili kuokoa wanandoa. Mafundisho ya kina yatolewe.
Wazazi wawafunde kwa kina wanandoa wachanga, msisitizo uwekwe wakati wa uchaguzi wa mwenzi. Lakini ... watu wamwogope kwanza Mungu. Usaliti, ukatili wa kijinsia na zinaa hutokana na kutoweka kwa hofu ya Mungu.
Ndoa inabakia kuwa ni tendo takatifu, tusiigeuze na kuwa chanzo cha vifo-maradhi- uwanja wa mateso na majuto.
0715-773366 |
May 4, 2012
NDOA NI NINI?
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment