MAKALA

Kubadilisha mawaziri hakutoshi, tubadilishe mfumo mzima


Elias Msuya
BAADA ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) Ludovick Utoh kuanika ufisadi wa kutisha wa Serikali, hoja kubwa imekuwa ni Rais kuwawajibisha mawaziri wanaoguswa.

Mawaziri wanaoguswa katika ufisadi huo ni pamoja na Waziri wa Fedha Mustapha Mkulo, Waziri wa Maliasili na utalii Ezekiel Maige, Waziri wa Nishati na Madini William Ngeleja, Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi) George Mkuchika, Waziri wa Uchukuzi Omar Nundu, Waziri Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Haji Mponda, Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Cyril Chami na Naibu wake, Lazaro Nyalandu.

Ripoti hiyo ya  CAG pia imeonyesha  kuwa deni la taifa limeongezeka kutoka Sh10.5 trilioni mwaka juzi na kufikia Sh14.4 trilioni mwaka jana.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo Serikali imetumia Sh 544 bilioni bila kuidhinishwa na Bunge, Sh bilioni moja zimelipwa mishahara kwa watumishi hewa na Sh 3bilioni zimetumika katika Balozi za Tanzania nje ya nchi ambazo ziko nje ya bajeti na misamaha ya kodi ya Sh1.02 trilioni.

Ripoti hiyo ilibainisha kuwa ripoti ya CAG kwa mwaka wa fedha ulioishia Juni 30,2010 inaonyesha Sh583.2 milioni zililipwa kama mishahara hewa, kiasi ambacho kingetosha kujenga madarasa 194.

   Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa LAAC, Augustino Mrema, kamati yake imebaini katika ripoti hiyo kuwa Sh8 bilioni  zilibainika kutumika katika manunuzi yasiyokuwa na nyaraka na ama yenye nyaraka pungufu hali inayoashiria kuwapo kwa wizi na kwamba kuna sh6 bilioni za miradi ya maendeleo hazijulikani ziliko.

Wakijadili katika kipindi cha Kipima Joto kinachorushwa na kituo cha Televisheni cha ITV hivi karibuni, Wabunge na wanaharakati wameshauri kubadilishwa kwa mfumo mzima wa Serikali tangu ngazi za chini ili kuondoa uozo uliopo.

Kwa upande wake Mbunge wa Mbozi Mashariki Godfrey Zambi anasema japo kila mwaka, taarifa za huko nyuma zilikuwa hazifikishwi Bungeni, lakini mwaka huu ililazimika kufikishwa.

Anaongeza kuwa licha ya kutofikishwa Bungeni, huko nyuma upotevu wa fedha haukuwa mkubwa kama ilivyo mwaka huu.

Huku akitoa mifano ya ubadhirifu, Zambi anasema japo hati za halmashauri mbalimbali zinaonekana kuwa safi, hali halisi ni mabaya.

“Kwa mfano tulikwenda kwenye halmashauri moja, darasa limejengwa kwa fedha za Tanapa lakini taarifa zinaonyesha kuwa zile ni fedha za halmashauri.

Lakini pia unakwenda Arusha kuna bwawa limetumia sh62 milioni lakini hazionekani kwenye hesabu. Taarifa za mwaka 2009/2010 ni mbaya, huko nyuma zilikuwa hazifikishwi Bungeni, ndiyo maana hata Rais alisema kama tumeshaunda mfumo huu basi ziende Bungeni.” anasema.
Akieleza jinsi wabunge walivyoshtushtushwa na ripoti hizo, Zambi anasema ni pale mabilioni ya fedha za miradi yanapoonekana yakipotelea kusikojulikana.

“Kwakweli lazima kama Mtanzania lazima ashtuke. Mimi kama Zambi niliyetumwa na Watanzania, niliyetumwa na wana Mbozi Mashariki niwasemee, sipaswi kunyamaza.”

“Ndiyo maana wabunge wa CCM tuliona vema tukae pamoja tusemane kwamba kwa hali hii siyo tuliyotumwa na wananchi. Tulikutana tukajadili na kukubaliana kuwa tumshauri rais aangalie upya wasaidizi wake. Namshukuru Waziri Mkuu ametusikia wamemshauri vizuri rais na leo kwenye vyombo vya habari tumesikia.”

Akitoa mfano mwingine wa ubadhirifu, Zambi anataja Halmashauri ya Kilosa ambako anadai kuwa kumna mtumishi aliyekuwa akiingiza fedha kwenye akaunti ya mpenzi wake, lakini adhabu aliyopewa ni kuhamishwa.

“Imefika mahali hali inaudhi sana, unafika kwenye Halmashauri ya Kilosa unakuta kuna mtu anafanyakazi ya kuingiza sh 200 milioni kweye akaunti ya ‘girlfriend’ wake, lakini hatua inayochukuliwa ni kuhamishwa kutoka Kilosa na kupelekwa kwingine.  Hata hapo Kishapu, kuna hela nyingi imepotea, kinachofanywa ni kuhamishwa kutoka halmashauri kwenda halmashauri nyingine.”


Nini kifanyike?
Mbunge wa Vunjo Augustine Mrema na Mwenyekiti wa kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) anasema kutokana na uozo uliojionyesha Rais anatakiwa kufumua mfumo wote wa Serikali na siyo Barza la mawaziri peke yake.

“Wabunge wameumizwa bila kujali itikadi zao za siasa. Wanataka mawaziri ambao wameshindwa kusimamia fedha wawajibishwe. Watu wasihamishwe, wakamatwe, washitakiwe,” anasema na kuongeza,

“Nchi hii imeoza, kama rais atafanya mabadiliko ya mawaziri, basi afanye na kwa makatibu wakuu ambako miradi yote inatokea, wakuu wa idara, kwa wakuu wa mikoa mpaka kwa wakuu wa wilaya makatibu tarafa na Kata mpaka kwenye jimbo, asafishe nchi hii.”

Ameongeza kuwa hali hiyo ndiyo iliwafanya wabunge waanzishe mkakati wa kupiga kura ya kutokuwa na imani na Waziri mkuu.

“Tunakwenda Bungeni pale, mawaziri hawawajibiki, makatibu hawawajibiki, hadi wakurugenzi wa maendeleo. Nashukuru baada ya kusoma taarifa ile Bunge limeridhia hatua zichukuliwe.” anasema Mrema.

Naye Godfrey Zambi anamuunga mkono Mrema akisema kuwa hatua hizo zisiishie tu kwa mawaziri, pamoja na kwamba mawaziri ni wakuu wa wizara, kwa kiutendaji wanaohangaika ni makatibu wakuu.
“Hatua hizi zisiishie tu kwa mawaziri kwani kiutendaji wanaohangaika ni makatibu wakuu.

Ukienda kwenye halmashauri wanaohangaika na mafaili ni wakurugenzi. Sasa kwa hali hii unaweza kubadilisha mawaziri ambao kweli wanahitaji kuwajibika, lakini bado wakaja mawaziri wengine wakashindwa. Wapo makatibu wakuu ambao hawaelewani na mawaziri wao.”

Zambi anaendelea kusema kuwa hatua za kubadilisha baraza la mawaziri zinaweza zisitibu tatizo kwani kuna mifumo mingi ya kubadilisha.
Anautaja mfumo wa sheria za nchi akisema kuwa unasaidia kulea uovu.

“Mfumo wetu wa sheria lazima ubadilike, ili mtu akionekana leo ameiba fedha za serikali ashughulikiwe mara moja. Mimi sidhani kama kuna mwingine mwenye utaalamu na hesabu kama CAG,” anasema na kuongeza,

“Mtu anaonekana kwenye taarifa ya CAG ametumia vibaya fedha za serikali, mara anasimamishwa kazi, kesi inakwenda mahakamani, mtu anakwenda mahakamani, mara kesi inakwenda kwa DPP mara imeenda huko na huko, inachukua miaka mitatu hadi minne, wakitafuta ushahidi.

“Huyu CAG yuko kisheria ameona yote kwenye vitabu kwamba hizi pesa zimeibiwa. Tunapofanya hivi tunamvunja nguvu huyu mdhibiti na mkaguzi wa hesabu za serikali.”

Zambi anashauri pia kwamba mtu anapobainika kuiba fedha za serikali, afilisiwe mali zake kwa sababu hakuzipata kihalali.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa asasi ya Fordia Bubelwa Kaiza anasema kiwango cha rushwa kwa Tanzania kimekuwa kwa asilimia 75 kutoka rushwa ya kawaida ya asilimia 45.

Hivyo anashuri kuwepo na mikakati ya muda mrefu na mifupi ikihusisha mamlaka za kisheria kama vile jeshi la polisi kuna Taasisi ya Kuzuia na kupambana na rushwa (Takukuru),  idara ya Usalama wa Taifa na mahakama.

“Kuna suala pia la taarifa katika vyombo hivi, kama tayari CAG ameshachunguza, taarifa zipelekwe haraka kwenye vyombo husika kama vile Takukuru wachukue hatua, kama suala linahusu Idara ya usalama wa taifa, taarifa ipelekwe haraka washughulikie. Rais anapopata taarifa asikie kuwa kuna watu wametuhumiwa, na hatua zimeshachukuliwa, siyo kama ilivyo sasa.”

Kaiza ameshauri pia kuchunguzwa kwa watu wanaopewa dhamana ya uwaziri ili kuepuka ubadhirifu kwa kuteua watu wasio waaminifu.

“Hawa viongozi wameingia madarakani kwa kupigiwa kura, tuangalie jinsi wanavyonunua kura, wanavyonunua wapiga kura wanavyofanya kila kitu ili kuingia madarakani,” anasema Kaiza na kuongeza;

“Halafu tuangalie jinsi Rais anavyoteua mawaziri, anavyowapata anajua, sijui nani anamshauri hakuna mahali popote wanapothibitishwa. Mawaziri wengine wamefeli hata mitihani lakini wamo tu, wengine tunawajua tunakutaka kwenye nyumba za wageni huko sasa sijui uadilifu uko wapi. suala la uadilifu ni la muhimu kwa watu wanaomsaidia rais”.

Kaiza anashauri pia kupunguzwa kwa madaraka ya rais ili wananchi wawe na mamlaka ya kuwawajibisha watendaji wa serikali wanaohujumu miradi ya Serikali.

“Nadhani kuna haja ya kubadilisha mfumo mzima, nadhani pia kuna haja ya kupunguza madaraka ya rais ili wananchi pate mamlaka yao. Hizo fedha zinazopelekwa kwenye halmashauri ili kutekeleza miradi zidhibitiwe na wananchi wenyewe. Wananchi ndiyo wenye miradi, wapewe mamlaka ya kuwawajibisha watendaji.”

“Vilevile vyombo husika vya sheria vitekeleze wajibu wake. Kama CAG anafanya kazi, Takukuru wanafanya kazi, jeshi la polisi nalo likifanya kazi na idara ya usalama nayo itafanya kazi, ubadhirifu wote huu hautatokea,” anasema Kaiza. 
                                                                                                                                                NA MWANANCHI     

No comments:

Post a Comment