Dec 19, 2011

DAWA YA MAPENZI

PAMOJA na kwamba wapo watu wengi waliofanikiwa katika suala zima la mapenzi, bado wapo vijana wa kiume ambao wamekuwa wakishindwa kuzikonga nyoyo za akina dada kutokana na kukosa maswali na majibu muafaka wanapokuwa wamewekwa kitimoto na watu hao wa jinsia tofauti, kwa nia njema ya kuweza kufahamiana na kujenga mahusiano.

Mara nyingi mazungumzo ya awali baina ya mwanamke na mwanaume huwa sawa na usaili wa kazi, huku mwanamke akiwa na maswali mengi zaidi kwa mwanaume, akijaribu kuepuka kuingia mkenge, hasa kama alipata kuumizwa au kuachwa kwenye mataa kwenye uhusiano wa kimapenzi siku za nyuma.

Baadhi ya vijana wa kiume, hususan wale waliolelewa katika maadili mema au utisho wa kidini, hutishwa na maswali ya akina dada na kujikuta wakishindwa kutoa majibu muafaka, hivyo kuwakosa akina dada hao. Unapomkosa msichana kwa sababu yoyote ile, ni wazi kuwa utaanza kujenga hofu unapokwenda kukutana na msichana siku nyingine. Ndiyo maana sasa unapaswa kufahamu maswali muafaka ya kuuliza na majibu muafaka kwa maswali ya mwanamke.

Wapo vijana ambao wangependa kufahamu kama kijana wa kiume naye anayo nafasi ya kumweka kitimoto msichana, hasa katika zama hizi za usawa wa jinsia ambapo wasichana wengi wamekuwa na hulka ya kujiamini na kujisimamia, ikilinganishwa na miaka ya nyuma kidogo. Pengine dukuduku haliishii hapo, kwani wapo wale watakaotaka kufahamu ni mambo gani muhimu ambayo kijana wa kiume anapaswa kumuuliza kijana wa kike, katika mkutano wao wa kwanza, au katika siku za mwanzo za mazungumzo yao.

Pia tunaweza kujiuliza, je, yapo maswali mafupi na marahisi ambayo mvulana anaweza kumuuliza msichana na kubaini kama ni msichana anayefaa kuwa mpenzi au mchumba, au ni changudoa? Kwa vyovyote vile, ni dhahiri kuwa ipo haja kwa vijana wa kiume ambao ndio wazungumzaji wakubwa katika uwanja wa mapenzi, kufahamu maswali muafaka wanayopaswa kuwauliza wale waliozigusa nyoyo zao na kuisisimua miili yao kiasi cha kuwafuatilia.

Kama ilivyoelezwa hapo juu, mara nyingi wanaume hujikuta wakitishwa na wanawake, kutokana na maswali yao magumu ambayo huwakatisha tamaa. Hii ni kwa sababu wanaume ndio hasa hujionesha kuwa wanataka kilicho uvunguni. Wanapobanwa kwa maswali na kukosa majibu muafaka, wanaume hawa hunyongea na kujikuta wakiziba midomo yao mapema kabla hata hawajafahamu mwanamke alimaanisha nini.

Lakini badala ya kukata tamaa mapema na kujikosesha mwanamke ambaye mwili wako husisimka na roho yako kupasuka mnapoonana, mwanaume anawajibika kujisimamia na kuchukua hatua, bila kujali kuwa mwishoni mambo yanaweza yasiwe mazuri.

Mwanamke anaweza kujiamini na kusimama kidete mithili ya mwanasheria wa Serikali aliyedhamiria kutetea ukweli, lakini hiyo haimaanishi kuwa mwanaume anapaswa kutetemeka na kunywea kama afanyavyo mtoto mdogo aliyepatikana na hatia ya udokozi.

Kuna njia mbalimbali ambazo mwanaume anaweza kuzitumia kukabiliana na hali hiyo ya kutisha na kukatisha tamaa. Njia mojawapo ni kuhakikisha kuwa unakuwa huru na kujiamini, huku ukiruhusu nguvu ya tabasamu na kicheko kutawala katika mazungumzo husika. Hakikisha kuwa tabasamu na kicheko chako haviwi vya bandia.

Lakini pia ni muhimu, kama ilivyosisitizwa, kuwa na majibu muafaka kwa maswali ya mwanamke. Mathalani, kama mwanamke atakuuliza, "Umewahi kuishi na mwanamke?" mweleze ukweli kuhusiana na maisha yako, ukisema, mathalani, "Ndiyo, nimepata kuishi na mke na nina mtoto mmoja." Baada ya hapo, yamkini utalazimika kueleza sasa unataka nini kwake ambapo pengine itabidi umhakikishie kuwa pamoja na historia yako hiyo, leo hii unampenda yeye.

Njia nyingine ya kukabiliana na shinikizo la mwanamke ni kukabiliana naye moja kwa moja na kujibu kila swali lake kwa jibu makini. Mathalani akikuuliza, "Ni kipindi gani kirefu zaidi ulichopata kuishi na mwanamke au kuwa na girlfriend?" mwambie ukweli papo hapo, mathalani kwa kusema, "Miaka mitatu. Vipi kuhusu wewe? Uliwahi kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mwanaume kwa kipindi gani?"

Pamoja na njia hizi, pia kuna maswali muafaka unayopaswa kuuliza na kuhakikisha kuwa unamshinda
mwanamke wako na kuiteka roho yake. Pamoja na kusaidia kumteka mwanamke, maswali hayo yatakusaidia pia kupata taarifa muhimu kuhusiana naye.

Unalopaswa kuzingatia zaidi ni kutokubaliana na kila jibu la kwanza unalopata kwa mwanamke kwa kila swali. Mara nyingi ukweli wa mwanamke hudhihirika unapomuuliza maswali kadhaa ya nyongeza kwa kila swali moja la msingi. Hapa lazima ujue kutumia maarifa ya bungeni katika kuuliza maswali ya nyongeza - mara nyingi hata bungeni maswali ya nyongeza ndiyo huwa na manufaa zaidi kuliko yale ya msingi.

Kwa hiyo, usiwe na papara ya kuuliza swali linalofuata, kabla hujapata majibu ya kuridhisha kwa
swali lililoulizwa. Pia zingatia kuwa wanawake wote ni wadadisi na watundu kwa asili. Mwanamke aliyeona thamani katika jinsia yake huuliza maswali magumu na ya kiudadisi kwa mwanamume anayemjia kwa ajili ya kumtaka kimapenzi.

Ni jambo zuri kwa mwanamke kuwa mdadisi kuhusiana na mwanaume anayemnyemelea, lakini ni dhahiri kuwa hakuna mwanaume anayependa kuona mwanamke akimpa shinikizo la damu kutokana na maswali yake. Ili kufanikiwa katika jambo hili, mwanaume anapaswa kutofautisha mwanamke mdadisi na mwanamke anayetaka mashindano. Mara nyingi hata kiimbo katika sauti ya mwanamke hubainisha msimamo wake, kama ni mdadisi au mtu wa shari anayetaka kukusasambua na kisha kukuachia maumivu na kuondoka zake.

Pia kuna jambo lingine muhimu kuhusiana na mawasiliano baina ya watu wa jinsia tofauti waliodhamiria
kupendana. Wanawake ni wasikilizaji wazuri zaidi kuliko wanaume na kwa hiyo vijana wengi wa kiume
hupaswa kujifunza sanaa ya kusikiliza, ili kujihakikishia kuwateka wanawake.

Kwa ujumla, mwanaume hupaswa kumuuliza mwanamke maswali ya kusisimua na yenye maana kuhusiana na yeye mwenyewe - maswali ambayo kuna kila dalili kuwa unataka kufahamu majibu yake na si kuuliza ilimradi tu.

Mojawapo ya malalamiko ambayo wanawake hutoa kuhusiana na wanaume ni kwamba wanaume huzungumza masuala yanayohusiana na nafsi zao tu na kushindwa kumuuliza mwanamke japo swali moja tu kuhusiana na nafsi yake. Jambo lingine la maana kabla ya kuyafahamu maswali muafaka ya kumuuliza mwanamke ni kuhakikisha kuwa huulizi maswali hayo bila kuwa tayari kujibu maswali mengine kama hayo kutoka kwake.

Mifano ya maswali ya kumuuliza mwanamke ambayo na wewe pia unapaswa kuwa na majibu yake ni kama vile, ni kosa gani kubwa ambalo unadhani wanaume hulifanya zaidi katika uhusiano wa kimapenzi? Swali hili ni muhimu kwa sababu litakubainishia ni kitu gani humuudhi zaidi mwanamke uliye naye, ili ukiepuke. Pia jibu lake hukupa taswira ya jumla ya mwanaume katika akili ya mwanamke unayezungumza naye.

Maswali mengine ni kama vile, Je, unawadhania wanaume kuwa waroho wa ngono au wenye kujali maslahi ya wanawake? Je, ni sifa zipi unazozidhania kuwa sifa za uhusiano wa kimapenzi unaopaswa kupigiwa mfano? Je, ulipata kuwa na uhusiano na mwanaume aliyekuwa changamoto kwako? (Mpe nafasi ya kueleza alikuwa changamoto kwa namna gani). Ni kitu gani muhimu zaidi katika mustakabali wa mapenzi?

Maswali mengine ya kumuuliza mwanamke ni kama vile je, uliwahi kuvunjika moyo kwa suala la kimapenzi? (Unapouliza swali hili omba kwamba jibu liwe 'ndiyo', kwani mwanamke aliyepata kuvunjika moyo ana roho ya upole na uvumilivu zaidi). Mengine ni je, ni kitu gani hukushtua unapokuwa unaelekea kufungua moyo wako kwa mwanaume? Je, katika mahusiano yako ya zamani na wanaume wewe ndiwe uliyewatema au wao ndio waliokutema?

Maswali mengine ni je, unadhani uliwahi kuwa na uhusiano wa kimapenzi wenye mafanikio? Je, ni kwa nini uhusiano wako wa mwisho wa kimapenzi na mwanaume ulivunjika?

Unapouliza maswali haya na mengine ya aina hii, kumbuka kuwa mwanamke anaweza kuja juu na kwa hiyo unapaswa kuwa tayari kumjibu. Kumbuka kuwa uhusiano wa kimapenzi ni kitu kinachohitaji kufikiria kwanza kabla ya kuchukua hatua na mara zote ni vema kumkosa mwanamke unapomtongoza kuliko akutose unapokuwa umemzoea.

HUU SI USAILI

Maswali haya ukiyauliza kwa mfuatano fulani utaonekana kama umemweka mwanamke katika usaili. Hali hii haitakupa alama zozote chanya na wala huwezi kujihakikishia kuwa utampata. Hakikisha kuwa maswali haya yanajitokeza kwa asili tu katika mazungumzo yenu.

No comments:

Post a Comment