May 3, 2012

UHURU WA VYOMBO VYA HABARI UMO HATARINI


Reporters without borders
Leo dunia inaadhimisha siku ya uhuru wa vyombo vya habari lakini uhuru huo umo hatarini katika sehemu kadhaa za dunia.

Mapinduzi yayolitokea katika nchi za kiarabu na za kaskazini mwa Afrika yameleta mabadiliko ya kina kirefu katika nchi hizo, lakini haina maana kwamba kazi ya waandishi wa habari imekuwa rahisi.

Msemaji wa mwenyekiti wa waandishi wa habari wasiojali mipaka, kanda ya Ujerumani Michael Rediske ameeleza kuwa mapinduzi yaliyotokea katika nchi za kiarabu yamesababisha mgogoro mkubwa.

Amesema waandishi wa habari wanapaswa kuwa ugani, lakini aghalabu wanashambuliwa, hasa na serikali zao.

Hata hivyo viwango vya uhuru wa vyombo vya habari vinatafautiana sana baina ya nchi na nchi. Kazi ya waandishi nchini Tunisia sasa siyo ya hatari kama ilivyokuwa hapo awali. Lakini nchini Syria waandishi wa habari kadhaa wameuawa tokea mapigano yaanze nchini humo. Mazingira yanayowakabili waandishi wa habari nchini Syria leo ni hatari sawa na yale yaliyojiri nchini Iraq katika miaka ya nyuma.

Hakuna waandishi wa kujitegemea Korea Kaskazini

Akisisitiza umuhimu wa kuiadhimisha siku ya leo ya uhuru wa vyombo vya habari duniani, msemaji wa mwenyekiti wa waandishi wasiojali mipaka , kanda ya Ujerumani bwana Rediske ameeleza:

"Ni siku ya kutanabahisha juu ya matatizo, juu ya hali ya uhuru wa vyombo vya habari, kwa kutilia maanani kwamba katika theluthi mbili ya nchi duniani, hakuna uhuru wa vyombo vya habari." Alitolea mfano wa Korea ya Kaskazini ambako hakuna waandishi wa kujitegemea, na kwa sababu hiyo hawakamatwi na Eritrea ambako waandishi wa habari wengi wanatiwa ndani.

No comments:

Post a Comment