May 17, 2012

USHOGA AMERIKA:PILIPILI USIYOILA YAKUWASHIA NINI?



Kwa Mukhtasari:
Yaliyokubalika juzi, yalikanwa jana, yaliyokanwa jana, yanakubalika leo. Rais Obama alipokubali ndoa za watu wa jinsia moja alifahamu kwamba jamii ya Amerika ina raia wa kila nui. Tunaomkashifu Obama ni wale tunaoomboleza zaidi kuliko waaliofiwa na tunaowashwa na pilipili iliyo shambani mwa jirani.
WATANZANIAna Waafrika wengi walionyesha kero na butwaa kufuatia tangazo kwamba Rais wa Marekani Barack Obama ameonyesha nia kuunga mkono haki za raia wa Amerika walio na mahusiano ya jinsia moja. Bila shaka mtazamo huo umekita mizizi kwenye imani kwamba uhusiano wa jinsia moja ni mwiko katika muktadha wa mila ya Kiafrika na ni dhambi katika mabano ya dini kuu ulimwenguni.
Makundi kadhaa  yalichukua jukwaa kukashifu hatua ya Rais Obama kana kwamba hatua ya Obama ni ukoma na ingewaangamiza kwa maradhi yasiyo na tiba. Isitoshe, ikumbukwe Rais Obama ni kiongozi wa Amerika na sioTanzania
 
Katika kukabili mabadiliko katika jamii haiwezekani kutumia itikadi na vifaa vilivyopitwa na wakati kupambana na changamoto za sasa. Ndivyo ilivyo tunapokumbana na suala kama ushoga lililo na utata kwenye nyoyo za watu wengi.
Iwapo msimamo wako unachochewa na dini, ni vema kutambua kwamba utakatifu wa tabia na mienendo sio jambo linaloweza kuendeshwa na sheria za umma hasa katika jamii ya imani zinazotofautiana. 
Yaliyokubalika juzi, yalikanwa jana, yaliyokanwa jana, yanakubalika leo. Mawimbi ya jamii hupanda na kushuka na ni sharti wanadamu wawe na wepesi wa kuyakubali angaa jamii iepuke kukuru kakara za migongano. Kuna mataifa yanayoendeleza hukumu ya kifo kwa kukatwa shingo, mengine yana hukumu hiyo hiyo kwa kuchanjwa sindano iliyo na sumu ilhali mengine kwa kitanzi shingoni.
Hukumu ya kifo
Kuna mataifa mengine yameonelea kuwa hukumu ya kifo kwa mbinu yoyote ile haileti haki kwa mhathiriwa; yaani kwa mwizi kuuawa, aliyeibiwa hanufaiki na chochote. Badaye, labda adhabu ya kufaa ingekuwa kumnyima tu uhuru katika jamii, kifungo cha maisha.
Suala la mapenzi ya jinsia moja ni mojawapo ya mambo ambayo hatuwezi kuwa na misimamamo inayokubalika kote na kwa wote. Hasa mjadawal mkuu ni ule wa swaji, Je, ni ushoga ni tabia ambayo mhusika ameichagua, kwa raha zake?  Au Je, ushoga ni suala la kimaumbile na mhusika amelipokea na kwalo hana uwezo kulibadili?
Uwezekano kwamba hali hii ni hali ya kimaumbile haupendezi wapinzani wengi wa haki za mashoga. Kwa sababu ya imani na tamaduni, mawazo ya wengi hayana fursa kutazama suala la ushoga katika mabano ya ‘ni kawaida’
Wengi wa wanaolaani mapenzi ya jinsia moja wanafanya hivyo kwa sababu finyu, sababu zilio ovu kimsingi. Wanateremea na kuona raha kwamba kuna watu wengi huko nje walio kwenye ‘dhambi’ mbaya kuliko zile zao. Kwa kutazama wengine kwa jicho la kuwakashifu, wengi wa watu wa aina hii wanajivunia kwamba hali zao ni kheri.
 Wanaopenda kukashifu tofauti watatafuta kila chembe cha tofauti kuzitumia kuendesha ubaguzi wao. Na hata kama tungechukua mkondo kwamba mashoga ni watu wasiotamanika katika jamii, ni lipi la kutenda kwa watu tusiokubali tabia zao, ilhali tabia zao hazituumizi kwa kwa lolote?
Hawawezi kujieleza
Tusichoweza kukataa ni kwamba kuna idadi kubwa ya raia hawa miongoni mwetu. Hata hivyo katika mataifa ya Afrika, ukosefu wa kuwakubali umewasukuma gizani hawawezi kujieleza au kujitambua; na kwa sababu wamezama na kufyata ndimi, Afrika inajinadi kwa dai ‘uhusiano kati ya watu wa jinsia moja si jambo la kiafrika’.
Hilo si kweli, uhusiano kati ya watu wa jinsia moja umekuwepo kwa karne kadha barani Afrika. Mahusiano hayo hata hivyo  hayakuwa mno ya kingono.
Tukikubali kwamba tunao kipengee hiki cha jamii, swali la pili ni lipi kuwatendea. Ustaarabu sio kuangamiza wale tusiopenda tabia zao, ustaarabu ni kuheshimu tofauti kati yetu, kuwaachia anga yao huku nasi tukipaa kwenye anga yetu. Katika kufahamu hilo jamii itaishi kwa uanana kwani haki itakuwa imetendwa.
Obama anafahamu kwamba jamii ya Amerika ina raia wa kila nui. Tunaomkashifu Obama ni wale tunaoomboleza zaidi kuliko waaliofiwa na tunaowashwa na pilipili iliyo shambani mwa jirani.

No comments:

Post a Comment