Apr 24, 2012

Raila anusurika ajalini Mombasa


Bw Odinga na Bw Mudavadi
Waziri Mkuu Raila Odinga (kushoto) na Naibu Waziri Mkuu Musalia Mudavadi wakiwa katika warsha ya serikali za mitaa awali. Picha/MAKTABA 
Na GALGALO BOCHA Na DANIEL NYASSY 
Kwa Mukhtasari
WAZIRI Mkuu Raila Odinga amenusurika baada ya msafara wake kuingilia ghafla na lori aina ya Canter kwenye barabara ya kuelekea uwanja wa ndege wa kimataifa wa Moi, Mombasa. Lori hilo lilimkosa kwa hatua chache.
WAZIRI Mkuu Raila Odinga Jumatatu alinusurika baada ya msafara wake kugongwa na gari la Canter barabara ya kuelekea uwanja wa ndege wa kimataifa wa Moi mjini Mombasa.
Kulingana na duru za polisi, msafara wa Bw Odinga ulikumbana na ajali hiyo pale ulipogongwa na gari hilo lililotoka upande wa pili na kumuumiza afisa wa polisi mwendeshaji wa pikipiki aliyemshindikiza Waziri Mkuu.
“Gari lilichomoza ghafla na kujitosa kwenye msafara kisha kumgonga mwendeshaji wa pikipiki likimkosa Waziri Mkuu kwa hatua chache,” alisema afisa mmoja wa trafiki aliyeshuhudia ajali hiyo.
Mkuu wa polisi mkoani Pwani Bw Aggrey Adoli alilaumu ajali hiyo kwa uendeshaji mbovu wa dereva wa Canter. Dereva huyo aliruka inje na kutoroka kwa miguu baada ya ajali hiyo na polisi kufikia Jumatatu jioni walikuwa wakimsaka bado.
“Tumeliburuta gari la Canter hadi katika kituo cha polisi cha Changamwe na tunamsaka dereva bado. Dereva huyo alijitokea tu kiholela upande wa pili pasipo kuangalia magaro mengine,” alisema Bw Adoli.
Bw Adoli alisema polisi mwendeshaji wa pikipiki alijeruhiwa kidogo na akaweza kuendelea na safari yake kuelekea uwanja wa ndege. Aliongeza kwamba pikipiki hiyo iliyokuwa ikiongoza msafara wa Waziri Mkuu iliharibika injini yake.
Kumjulia hali
Bw Odinga alishuka kutoka kwa gari lake na kuenda kumjulia askari huyo hali yake huku msongamano mkubwa wa magari ukitokea pande zote za barabara huku polisi wakijaribu kuivuta Canter hiyo kuelekea kituo cha polisi cha Changamwe.
Baadae, msafara wa Waziri Mkuu uliendelea hadi uwanjani mwa ndege na waziri Mkuu kuendelea na safari yake ya Nairobi.
“Waziri Mkuu alisimama pale kwa takriban nusu saa akiongea na maafisa wa polisi akiuliza hali ya mwenzao. Kisha alirejea ndani ya gari lake na wakaenda,” askari aliyeshuhudia kisa hicho aliliambia gazeti la Taifa Leo.
Bw Odinga alikuwa akirudi Nairobi baada ya ziara ya siku mbili mkoani Pwani ambapo alihudhuria harusi ya mwanaharakati wa haki za binadamu Bw Hassan Omar Sarai ambaye pia ametangaza kuwania kiti cha useneta wa kaunti ya Mombasa.

No comments:

Post a Comment