May 9, 2012

MTOTO ACHOMWA KWA KUMPA JIRANI SUKARI


sukari
Kwa Mukhtasari
Mama wa watoto wawili eneo la Bomet nchini KENYA anadaiwa kumchoma mwanawe wa miaka saba akitumia kisu alichokipasha moto kwa kumpa jirani vijiko viwili vya sukari.

MAMA wa watoto wawili ameshtakiwa katika mahakama ya Bomet kwa madai ya kumchoma mwanawe wa miaka saba kwa kumpa jirani vijiko viwili vya sukari.
Ilisemekana Bi Nelly Chelagat alimjeruhi mtoto huyo kwa kumchoma akitumia kisu alichokipasha moto, katika mtaa wa Zebra mjini Bomet.
Alishtakiwa Jumatano kwamba katika siku tofauti mwaka huu, alikitia kisu kwenye moto na kuuchoma mgongo wa mtoto huyo kama njia ya kumtia adabu, alipogundua kuwa mtoto huyo alikuwa mkarimu kwa jirani.
Akisimamishwa kizimbani mbele ya Hakimu Mkazi wa wilaya ya Bomet Bi Virginia Karanja, Bi Chelagat alikanusha mashtaka hayo. Inasemekana kuwa mama huyo alipandwa na hasira alipogundua kwamba bintiye alimchotea jirani sukari bila kujali gharama ya maisha.
Baada ya kisa hicho, polisi wa utawala wakiandamana na chifu wa eneo hilo Bw Reuben Ngetich, walimkamata mshtakiwa na kumpelekea hadi kituo cha polisi ambako alifunguliwa mashtaka ya kumtesa mtoto wake.
Alipokanusha shtaka hilo, mshtakiwa ambaye hakuwasilisha ombi la kuachiliwa kwa dhamana, alipelekwa katika rumande ya gereza la  Kericho hadi wiki ijayo.
Kufa maji
Kwingineko, mwanaume anayefanya kazi ya umekanika alifariki kwa kufa maji akijaribu kuokoa kofia yake. Polisi wa Gatundu Kusini wanautafuta mwili wa mwanaume huyo wa miaka 26, aliyetumbukia katika Mto Thiririka.
Mkuu wa polisi wa Gatundu Bw Peter Kattam alisema kuwa mekanika huyo aliyetambuliwa kwa jina la Simon Gitau, alikuwa akienda zake nyumbani kutumia bodaboda mwendo wa saa mbili unusu usiku.
Akiwa amebebwa nyuma ya pikipiki, walipofika daraja la Thiririka, upepo mkali uliichomoa kofia kichwani mwake.
“Alimuomba mwendeshaji bodaboda asimamishe pikipiki ili aifuate kofia yake. Aliteleza na kutumbukia kwenye mto huo uliofurika kutokana na mvua inayoendelea kunyesha,” alisema Bw Kattam.
Mwendeshaji bodaboda alijaribu kumwokoa abiria wake lakini mawimbi mazito ya maji ya mvua yakamzuia kumfikia.

No comments:

Post a Comment